Friday, December 27, 2013

HUU NDIO UCHUNGU WA WATUMWA WEUSI WALIOKUWA WAKIFANYIWA BABU ZETU HUKO MAREKANI INAUMA SANA....!!















As-Salamu Alaykum wapenzi wasomaji wa Makala ya Wiki ambayo inaangazia ukandamizaji na mateso makali yaliyofanywa na watu weupe wa Magharibi dhidi ya watumwa weusi huko Marekani. Karibuni….
Historia ya watu weusi nchini Marekani imejaa mashaka na misukusuko na  machungu mengi. Asili na chimbuko aghlabu ya Wamarekani weusi nchini humo, inarejea barani Afrika. Kwa miaka mingi iliyopita mababu wa watu hao walitekwa na Wamarekani kutoka Afrika na kupelekwa nchini humo katika hali ya kinyama na wakalazimishwa kuwa watumwa. Bila dhambi wala kosa lolote, watu hao walifanywa watumwa na kudunishwa na kudhalilishwa sana kwa sababu tu ya rangi ya miili yao. Tangu wakati huo watun hao waliishi kwenye mashaka na matatizo makubwa na hawakuonja tena ladha ya maisha mazuri.

Japokuwa hivi sasa rais wa Marekani ni mtu mweusi, lakini inatupasa kuelewa kuwa Barack Obama ni mwakilishi wa jamii ndogo sana ya watu weusi wenye maisha bora nchini humo na ambao walipata kuingia serikalini kupitia fursa maalumu. Utumwa nchini Marekani ulianza mwaka 1691 na biashara ya kuwaingiza nchini humo watumwa kutoka Afrika ilianza katika karne ya 17 na 18. Watumwa hao walikuwa wakitumikishwa katika mashamba ya tumbaku, mpunga, pamba na mahindi na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya Marekani. Kwa kawaida kazi ngumu sana kupita kiasi zilikuwa zikitendwa na watumwa. Hata hivyo walikuwa wakipewa mshahara kiduchu sana ukilinganishwa na jamii ya weupe.
Kama hiyo haitoshi, watumwa wa kike wajawazito nao walikuwa wakilazimishwa kufanya kazi ngumu katika mashamba. Wanawake hao walikuwa wakitakiwa kuwanyonyesha watoto wao kwa kipindi cha miezi mitatu hadi minne tu, jambo ambalo lilipelekea karibu nusu ya watoto weusi kufariki dunia. Hivi ndivyo alivyokuwa Mmarekani tunayemfahamu hii leo na ambaye anajinadi kuwa mtetezi wa haki za binadamu duniani. Ukweli ni kwamba, uti wa mgongo wa uchumi wa Marekani na shughuli zote za kimaendeleo, vimejengwa na nguvu za watumwa ambao hii leo hata hakuna anayewakumbuka huku wajukuu wao wakiendelea kubaguliwa kila uchao.
Alex Haley ambaye naye ni mtu mweusi na mwandishi mkubwa wa Kimarekani, anaelezea vizuri katika kitabu chake cha Roots mateso yaliyowakumba watumwa kutoka Afrika na mtu yeyote anayesoma kitabu hicho atapatwa na uchungu na simanzi kutokana na mateso na unyanyasaji mkubwa uliofanywa dhidi ya Waafrika hao. Kitabu cha Roots kinaanza kuelezea maisha ya mmoja kayi ya mababu wa Alex Haley mwenyewe kwa jina la Kunta Kinte. Kunta Kinte ni babu wa saba wa mwandishi wa kitabu hicho ambaye aliletwa Wamarekani kutoka Gambia kulazimishwa kuwa mtumwa.

****************************************
Simulizi za kitabu hicho zinaanzia mahali panapoitwa Juffure huko nchini Gambia. Gambia ni nchi iliyoko magharibi mwa Afrika na uchumi wake unategemea kilimo, uvuvi na utalii. Kisa cha kitabu cha Roots kinaanza kwa kuzungumzia mazazi ya Kunta Kinte na sherehe za kupewa kwake jina hilo. Alex Haley anaanza kuzungumzia tamaduni wa watu wa asili yake mwenyenye kuanzia kwenye sherehe hizo. Baba wa Kunta Kinte alikuwa Mwislamu ambaye alichunga na kuheshimu thamani za dini hiyo wakati wa kumpa jina mtoto wake mchanga.

Kunta alikulia katika mazingira mazuri ya Kiafrika. Baba yake alimpa uhuru kamili wa kufanya kazi huku mama yake akifanya jitihada kubwa katika kumpa malezi mazuri. Baba alimsisitiza sana kushikamana na Sala na kuienzi ibada hiyo. Kwa hakika mafunzo ambayo baba alimpatia mwanaye yalikuwa yamejaa ukweli na adabu za hali ya juu. Alikatazwa tabia ya kusema uongo na na kufunzwa jinsi ya kuwaheshimu watu wakubwa.

Siku moja Kunta Kinte alipokuwa amekwenda kutafuta mbao kwa ajili ya  kutengenezea ngoma ya ndugu yake, alijikuta katika mikono ya watu weupe na huo ndio uliokuwa mwisho wa maisha matamu ya ujana wake. Baada ya watu hao weupe kumkamata walianza kumpiga na baada ya mateso makali walimuweka katika jahazi lililokuwa na uvundo na kupelekwa Marekani. Wakati huo mwili wake licha ya kuwa hoi kutokana na mateso makali, uliendelea kuteseka kutokana na minyororo aliyofungwa miguuni na mikononi. Kunta alipata maumivu makubwa zaidi kutokana na chuma alichokuwa amewekewa mabegani katika kipindi chote cha safari ndani ya jahazi hilo.
Katika kipindi chote cha safari Kunta Kinte alikuwa akijiuliza kwa nini watu weupe wanafanya ukatili mkubwa kiasi hicho? Alijisemeza mwenyewe kwamba, yumkini watu weupe hawana Mungu, kwa sababu hawaheshimu chochote na hawakuwaonea huruma hata wanawake weusi?
Kitabu hicho cha Roots kina picha za kusikitisha mno za ndani ya jahazi lililotumika kusafirisha watu wa Kiafrika kuelekea Marekanihatimaye kijana huyo wa Kiafrika aliouzwa kwa mabwana wa Kizungu. Kunta alijaribu kutoroka mara nne kutoka katika mikono ya watu hao weupe na mbwa zao lakini juhudi zake ziligonga mwamba.

XXXXXXX
Kwa mujibu wa sheria za wazungu hao makatili, ikiwa mtu mweusi atatazama katika uso wa mtu mweupe, basi alikuwa akitandikwa mboko 10. Aidha sehemu nyingine ya sheria za wazungu hao ni kwamba, ikiwa mtu mweupe ataapa kupinga maneno yaliyosemwa na mtu mweusi, basi ana haki ya kumkata sikio lake moja. Ikiwa mweupe atasema kuwa, mtu mweusi amesema uongo kwa mara ya pili, basi ana haki ya kukata sikio lake la pili. Sheria hizo za kidhalamu zinasema kuwa, ikiwa utamuua mtu mweupe, basi hukumu yake ni kunyongwa na ikiwa utamuua mtu mweusi mwenzako, adhabu yake ni kutandikwa mijeledi. Kusoma na kuandika kulikuwa haramu na marufuku kwa watu weusi. Vilevile kuwapa kitabu watu weusi lilikuwa kosa na kinyume na sheria. Hayo ni sehemu ya maneno ya mtu mmoja mweusi katika simulizi za kisa cha Kunta Kinte. Baada ya Kunta kujaribu kutoroka mara nne na kukamatwa wazungu makatili waliamua kukata sehemu ya mguu wake wa kulia ili asijaribu tena kuchukua hatua hiyo. Viganja vya mikono ya watu weusi vilipigwa misumari kwenye kuta na walikuwa wakilazimishwa kula na kutafuna masikio yao yaliyokatwa na wazungu.

XXXXXX
Licha ya baadhi ya filamu za Marekani zinazowaonyesha watu weusi kuwa wakatili na wala watu, kitabu cha Alex Haley kinamuarifisha mtu mweusi kuwa ni mtu aliyestaarabika kwa mafundisho ya Qur’ani Tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad (saw). Kinamtangaza mwafrika kuwa ni mtu muungwa. Mara zote Wamagharibi na Wamarekani, wanafanya propaganda za kuwaarifisha watu weusi kuwa hawana ustaarabu na kwamba ni watu wa mwituni ambao wamestaarabishwa na kuneemeshwa na watu weupe. Haley katika kitabu chake cha Roots, amebatilisha madai kwamba watu weusi hawakuwa watu waliostaarabika. Kitabu hicho kinaweka wazi ukweli kwamba, watu weusi hawakupenda kuwaona watu weupe bali hata kunusa harufu yao.

XXXXXXX
Kitabu cha Roots kinaendelea kusimulia kisa cha matatizo na mashaka ya Kunta Kinte na mambo yaliyovipata vizazi vya baadaye hadi wakati wa mwandishi wa kitabu hicho Alex Haley. Haley alitumia muda wa miaka 12 katika kufuatilia historia ya mababu zake wa Kiafrika. Kwa hakika kisa cha Roots kinavutia sana. Pamoja na kitabu hicho kuwa na kurasa 700, lakini kinamfanya msomaji asikiweka chini bila ya kukimaliza. Kitabu hicho (Roots) kilichapishwa mwaka 1976 na nakala milioni moja na laki tano zilikuwa zimeuzwa katika kipindi cha chini ya miezi saba tu sambamba na kujipatia zawadi kemkem. Hivi sasa kitabu hicho kimetafsiriwa katika lugha 37 za dunia. Zaidi ya hayo mwaka 1977 na 1979 kulitengenezwa filamu mbili muhimu na zilizopata watazamaji wengi nchini Marekani, kwa mujibu wa na kisa na simulizi za kitabu hicho na kuonyeshwa na kanali ya ABC ya Marekani.


Kisa hicho kinaelezea ukatili na dhuluma za kuchupa mipaka za watu weupe wa Magharibi dhidi ya watumwa kutoka Kiafrika. Familia ya Alex Haley ilikuja kupata ahuweni baada ya kumalizika vita vya ndani nchini Marekani, yaani mwaka 1861-1865 Miladia. Hata hivyo hali haikuwa nzuri kwa watumwa wengine wa Kiafrika nchini Marekani. Katika kipindi cha kati ya miaka 1880-1890 Wafrika walikuwa wakiuawa kwa kuchomwa moto wakiwa hai, au kukatwakatwa au kutundikwa juu ya miti hadi kufa. Vitendo hivyo havihusiani na zama za mwanadamu kabla ya historia bali ni matukio ambayo yametokea katika kipindi cha miaka 120 hadi 130 tu iliyopita nchini Marekani.    
XXXXXXX

Alireza Farahmand mfasiri wa kitabu cha Roots kwa lugha ya Kifarsi anaandika hivi katika utangulizi wake: “Mizizi daima umekuwa sehemu isiyoonekana, muhimu na yenye manufaa zaidi katika mti. Mizizi katika riwaya ya Alex ni watu weusi na watumwa kutoka Afrika ambao walistawisha na kukuza mti wa uhuru wa adhama ya uchumi wa Marekani na kuufikisha hapa ulipo. Hata hivyo inaikitisha kuwa, kadiri mizizi hiyo ilivyokita chini ya udondo ndivyo wazungu walivyokuja juu na matawi na majazi ya mtu kuchanua zaidi. Inaumiza sana kuona kwamba wakulima halisi wa bustani ya miti hiyo hawakuruhusiwa kula hata tunda moja la bustani hiyo….    

                                                             

MPENZI MSOMAJI TUPE MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII HAPA CHINI

SHARE HABARI HII KWA RAFIKI ZAKO HAPA CHINI==>>

KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU BASI BOFYA "LIKE" HAPO CHINI KUUNGANA NASI KWENYE FACEBOOK.

0 comments em “HUU NDIO UCHUNGU WA WATUMWA WEUSI WALIOKUWA WAKIFANYIWA BABU ZETU HUKO MAREKANI INAUMA SANA....!!”

Post a Comment

 

Mambomseto Blog Copyright © 2011 -- Template created by SKENDO TEAM -- Powered by SKENDO TEAM

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter