Wednesday, December 25, 2013

MAUAJI KRISMASI


INATISHA sana! Msimu wa Sikukuu ya Krismasi umekuwa mchungu kwa familia ya Diwani wa Kata ya Nkangamo, Tunduma jijini hapa, Weston Simwelu (55) baada ya mwanaye Kalebu Simwelu (6) pamoja na hausigeli wao kuchinjwa kikatili kama kuku huku mtuhumiwa namba moja akiwa ni mwanaye mkubwa, Enock Simwelu (23).

Habari zilieleza kuwa familia hiyo ilikumbwa na mkasa huo Desemba 20, mwaka huu wakati ikijiandaa na sherehe ya Krismasi ambapo mtuhumiwa alidaiwa kukiri kuhusika na mauaji hayo.

CHANZO NI NINI?
Katika mahojiano na polisi baada ya kukamatwa, Enock alidai kuwa chanzo cha yote ni kitendo cha baba yao huyo kumrithisha mali zote marehemu mdogo wao, Kalebu.

WAFICHA MIILI
Awali ilielezwa kuwa, siku ya tukio, mtuhumiwa akiwa na wenzake wawili, akiwemo mmoja aitwaye Gabriel walivamia nyumbani kwa diwani huyo na kufanya mauaji ambapo walimchinja kwa kisu mtoto Kalebu na mfanyakazi wa ndani aliyetajwa kwa jina la Sista Nyirenge (17). (kama kisa ni mali yeye alikosa nini, au walijua atawataja?).


Kama vile ukatili huo haukutosha, habari zinadai kwamba baada ya kuwachinja marehemu hao na kuhakikisha wamekata roho, waliificha miili yao sebuleni nyuma ya kochi wakiamini itakuwa vigumu kupatikana (si rahisi maiti isionekane sebuleni).


Iliendelea kudaiwa kuwa, Enock pamoja na wenzake ambao ni nduguze wa mama mmoja, walishirikiana kutekeleza ukatili huo kwa madai ya kwamba baba yao alifanya upendeleo wa kumrithisha mali mdogo wao ambaye ni mtoto wa mke mdogo wa diwani huyo (hapa pana maswali mengi).

KAMANDA ATHIBITISHA KUTOKEA KWA MAUAJI
“Chanzo cha mauaji hayo kimebainika, mtoto wa mke mkubwa wa diwani, Enock amekiri kuhusika na mauaji hayo akishirikiana na nduguye aitwaye Gabriel Simwelu.


“Madai yao ni kwamba baba yao alimwandikisha mali zote marehemu Kalebu, mtoto wa mke mdogo wa diwani, ikawauma,’’ alisema Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakael Masaki.


Kwa mujibu wa Kamanda Masaki, mmoja wa watuhumiwa walioshikiliwa ni kaka wa marehemu, Enock ambaye ataisaidia polisi katika upelelezi wa tukio hilo la kutisha kabisa katika siku za hivi karibuni.
Kamanda Masaki alisema kuwa mauaji hayo pia yalifanywa kwa kushirikiana na jirani na rafiki yao aliyefahamika kwa jina la Patrick Msigwa (18), mkazi wa eneo la Majengo katika mji mdogo wa Tunduma.


Mara baada ya kutokea kwa mauaji hayo jeshi la polisi liliwanasa watu watano wakiwemo watoto wa mke mkubwa wa Diwani Simwelu.

WAZAZI WALIKUWA WAPI?
Wakati tukio hilo la mauaji linatokea, baba wa marehemu Kalebu, alikuwa shambani katika Kijiji cha Kipaka huku mama mzazi aitwaye Tumaini Yohana (29) akiwa kazini katika Ofisi ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Wote walipelekewa taarifa ambapo mama huyo inadaiwa alishindwa kuvumilia na kupoteza fahamu (hata ungekuwa wewe).

MASHUHUDA WANASEMAJE?


Wakizungumza kwa masikitiko na gazeti hili, mashuhuda wa tukio hilo walisema wamesikitishwa na tukio hilo ambalo limetibua shamrashamra zote za Krismasi kwa familia hiyo na majirani zao.

“Jamani watu tumejiandaa kwa sherehe halafu linatokea tukio baya kama hili. Familia ya Simwelu ndiyo kabisa haina hata hamu na hiyo sikukuu,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye alikuwa akimwaga machozi kwa uchungu.


WALIKOZIKWA MAREHEMU
Marehemu Kalebu alizikwa kwenye Makaburi ya Nakonde, mji mdogo uliopo nchini Zambia na kuhudhuriwa na umati wa wakazi wa mpakani mwa Tanzania na Zambia (haijajulikana sababu).

Mazishi ya mfanyakazi wa ndani, Sista Nyirenge yalifanyika katika Kijiji cha Isansa wilayani Mbozi, Mbeya.
Mungu aziweke pema peponi roho za marehemu wote. Amina.

-gpl 

MPENZI MSOMAJI TUPE MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII HAPA CHINI

SHARE HABARI HII KWA RAFIKI ZAKO HAPA CHINI==>>

KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU BASI BOFYA "LIKE" HAPO CHINI KUUNGANA NASI KWENYE FACEBOOK.

0 comments em “MAUAJI KRISMASI”

Post a Comment

 

Mambomseto Blog Copyright © 2011 -- Template created by SKENDO TEAM -- Powered by SKENDO TEAM

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter