Tuesday, January 7, 2014

Mwanamke wa kitanzania anaswa na Madawa ya Kulevya Uwanja wa Ndege Dar akiyapeleka Macau nchini China


KIKOSI cha Kuzuia na Kupambana na dawa za kulevya nchini, kimemkamata mwanamke mmoja Mtanzania akiwa amebeba kete 63 za dawa za kulevya aina ya heroine. 

Mwanamke huyo, Salama Mzara mkazi wa Mbagala, jijini Dar es Salaam, alikamatwa juzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akiwa njiani kuelekea Macau nchini China.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kikosi hicho, Godfrey Nzowa alisema, kikosi kazi kilichopo uwanjani hapo kilimkamata Mzara mwenye umri wa miaka 39 juzi saa 10 jioni, baada ya kumuhisi kubeba dawa za kulevya.

“Alipofika uwanjani wakati wa kukaguliwa walimuhisi atakuwa amebeba dawa za kulevya, ndipo walipoamua kumchukua na kwenda kumuhoji, baada ya kumuhoji ilibainika amemeza dawa hizo na ameweza kutoa kete 38 za heroine,” alisema Kamanda Nzowa.

Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anajiandaa kupanda ndege ya shirika la ndege la Ethiopia (Ethiopia Airline) kuelekea Macau kupitia Addis Ababa.

Kwa mujibu wa Nzowa, alidai kuwa msichana huyo bado anaendelea kuhojiwa na kwamba utaratibu wa kumtaka kuendelea kuzitoa kete alizomeza unaendelea, kwani anaonekana amebeba mzigo mkubwa zaidi.

“Mzigo alioutoa ni mdogo hawezi kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kupeleka mzigo huo tu.

“Bado tunaendelea kumuhoji, lazima atakuwa na kete nyingine zaidi, kete alizozitoa ni ndogo hawezi kwenda nje ya nchi na kete 38 ni chache sana, tunaamini tunavyoendelea kukaa naye atatoa zaidi ya hizi,” alisema Kamanda Nzowa.

Nzowa alisema kwa sasa watu wengi wanaosafirisha dawa za kulevya wanatumia zaidi usafiri wa anga baada ya kudhibitiwa bandarini, kwakuwa mwaka jana waligundulika kutumia zaidi njia ya maji na wengi wao walikamatwa bandarini walipokuwa wanataka kusafirisha dawa hizo.

Aidha pia wamefanikiwa kumkamata raia mmoja wa Nigeria, Okwudila Mnamani akiwa na kete 71 za dawa za kulevya, mtu huyo alikamatwa Desemba 29, mwaka jana, ambapo jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kujibu tuhuma hizo za kukutwa na dawa hizo.

Nzowa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa akijaribu kupita katika uwanja huo kwa ajili ya kuelekea nchini Uholanzi, ambapo alikuwa amezimeza kete hizo.

Kukamatwa kwa mwanamke huyo kunaendeleza wimbi la wanawake wa Tanzania kutumika katika kusafirisha dawa hizo, ambapo katika kipindi kifupi zaidi ya wanawake watatu wameshakamatwa nje ya nchi wakisafirisha dawa hizo.

>>Mtanzania 

MPENZI MSOMAJI TUPE MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII HAPA CHINI

SHARE HABARI HII KWA RAFIKI ZAKO HAPA CHINI==>>

KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU BASI BOFYA "LIKE" HAPO CHINI KUUNGANA NASI KWENYE FACEBOOK.

0 comments em “Mwanamke wa kitanzania anaswa na Madawa ya Kulevya Uwanja wa Ndege Dar akiyapeleka Macau nchini China”

Post a Comment

 

Mambomseto Blog Copyright © 2011 -- Template created by SKENDO TEAM -- Powered by SKENDO TEAM

Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter